Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mh. Shaibu Ndemanga amewaonya wananchi wanaofanya shughuli zao karibu na Misitu ya jamii kuacha mara moja tabia ya kuchoma moto mashamba kwaajili ya maandalizi ya shughuli za kilimo kwani hii inasababisha misitu mingi kuungua na kurudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau waliojitoa katika upandaji na usimamizi wa misitu hiyo.
Ndemanga, Ameyasema hayo Novemba 6,2021 katika ziara yake ya kukagua Mradi wa Kuongeza Usimamizi wa Misitu ya Jamii unaotekelezwa na Shirika la Usimamizi wa Misitu Asilia TFCG katika Kata ya Namupa Halmashauri ya wilaya ya Mtama mkoani humo.
Aidha, amewataka wananchi hao kuacha kilimo cha kuhamahama, kuendeleza shughuli ndani ya hifadhi na kusisitiza uwepo wa usimamizi shirikishi katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kijijini hapo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi Ndg. Thomas Safari, Afisa utumishi wa Halmashauri ya Mtama Ndg. Mahmoud Kimbokota pamoja na baadhi ya Wataalamu kutoka Idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.
Ndemanga, alianza kupokea taarifa za maendeleo ya Mradi iliyotolewa na Meneja wa Mradi Bw. Yahaya Mtonda katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri pamoja na kutembelea Vijiji vilivyofikiwa na Mradi huo. Alitembelea msitu na kitaru cha miti kinachosimamiwa na kikundi cha kuweka akiba cha Namupa chenye miche iliyoota jumla ya 1600. Akiwa kwenye kitaru hicho Mkuu wa Wilaya aliwapongeza wanakikundi hao na kuwashauri waongeze juhudi kupanda miti ya asili kama vile mipingo, mibambakofi na mninga.
Kupitia ziara hiyo, aliupongeza uongozi wa TFCG kwa kufanikiwa kupeleka mradi katika Wilaya ya Lindi hususani kwenye vijiji vya ukanda wa Rondo kwani utasaidia kutunza vyanzo vya maji pamoja na uoto wa asili. Aidha aliwaomba watu wa Shirika hilo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza misitu ya hifadhi yenye wanyama pamoja na kuongeza juhudi kubwa za kupanda miti ya asili iliyopotea kwenye misitu mbalimbali ili iwe fursa kwao kuongeza vivutio vya utalii.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika hilo Wilaya ya Mtama Bw. Yahaya Mtonda ameeleza ya kuwa shirika limeamua kuanzisha mradi huo ili kuhimiza utunzaji na uongezaji wa misitu kutokana na uharibifu unaopelekea kusambaa kwa wanyama kama vile Tembo wanaovamia maeneo ya shughuli za binadamu hususani kwenye vijiji vya Rondo na kwamba kwa kufanya hivyo kutaimarisha na kuwafanya wanyama hao kubaki katika makazi yao.
Mtonda aliongeza kuwa mradi huo pia unasaidia kuanzisha vikundi vya kujasiliamali kama vile ufugaji wa kuku pamoja na vikundi vya kuweka akiba ili kujikwamua kiuchumi. Aidha mradi huo utahakikisha unaanzisha viaru vya miti ikiwa ni mikakati ya kuendeleza hamasa za uongezaji wa misitu
Katika kuhakikisha misitu inatunzwa na kupunguza migogoro ya ardhi vijijini, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Victor Shau ambaye amezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtama, amesema yakuwa Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wa maendeleo itahakikisha misitu yote inatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Lakini pia ametoa rai kwa uongozi wa vijiji na Kata kutumia kikamilifu sheria ndogo za Mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Muungao II Kata ya Namupa Rafael Milanzi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Shirika la Usimamizi wa Misitu Asilia kwa kusaidia kuondoa migogoro ya mipaka ya Chiwerere-Muungano, Nndawa-Muungano pamoja na Namupa-Muungano. Lakini pia kijiji kimefanikiwa kutenga msitu wa nyongeza wenye hekta 525 huku akiuomba uongozi wa mradi kukamilisha taratibu ili msitu huo uweze kutangazwa kwenye gazeti la Serikali kuwa kama kivutio cha utalii.
Mradi huo unaofadhiliwa na World Land Trust ulianza rasmi Julai 2020 na unatekelezwa kwa muda wa miaka 3. Mpaka sasa mradi umevifikia takribani vijiji 10 ambavyo ni Ntene, Chiodya, Namupa, Liganga, Mihima, Nndawa, Chiwerere, Muungano II, Mnamba na Mnara. Mradi umefanikiwa kuanzisha misitu ya hifadhi katika vijiji 8 vyenye jumla ya hekta 17376.91, kuwezesha kuanzisha shughuli za ufugaji wa kuku kupitia vikundi vinavyoendeshwa na mfumo wa vikoba ambapo jumla ya kuku 1033 wamesambazwa, pamoja na kuondoa migogoro ya mipaka ya ardhi kwenye vijiji mbalimbali vya mradi huo.
Dc Ndemanga akiwa kwenye kitaru cha miti Namupa
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.