Halmashauri ya Wilaya Mtama imetoa mikopo yenye thamani ya Tshs. 59,600,000/= kwa vikundi 21 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Mikopo hiyo imetolewa tarehe 15 Novemba 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga katika viwanja vya Halmashauri hiyo.
Akikabidhi pikipiki na fedha kwa vikundi hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga aliwataka wajasirimali walikopa kuhakikisha kwamba wanafanyia kazi zilizokusudiwa ili kujiinua kimapato na kurejesha fedha hizo ili zitumike kuwakopesha wengine.
Vilevile aliwataka vijana wa bodaboda kutumia pikipiki hizo kujiinua kiuchumi na si katika anasa na kuwarubuni wanafunzi hali ambayo Serikali haitawafumbia macho katika suala hilo.
"Tumewapa mikopo kuchukua abiria, hao wanafunzi ni abiria acheni kutumia pikipiki kama chambo kwa watoto wa shule. Tunawatakeni muwaache watoto wa shule wasome na watimize ndoto zao" alisema Ndemanga na kuongeza kuwa wakibaini wanatumia pikipiki hizo katika uhalifu wa aina mbalimbali ukiwemo kurubuni watoto wa kike watawapokonya.
Kutokana na kuwepo kwa changamoto za ongezeko la mimba za utotoni zinazosababishwa na madereva wa bodaboda Mhe. Ndemanga amesema kuwa wao wataendelea kuwaangalia kwa jicho kali kuona kwamba hawatumii rasmimali hizo kuwakwamisha wanafunzi.
Akisoma taarifa fupi ya mikopo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, George Mbilinyi alisema vikundi 8 vya vijana vimekopeshwa pikipiki, vikundi 10 vya wanawake na vikundi 3 vya wenye ulemavu vilikopeshwa fedha.
Aidha Mbilinyi alieleza kuwa katika kipindi cha Robo ya Kwanza Mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya Mtama imetoa Mikopo yenye thamani ya Tshs. 59,600,000/= kwa vikundi 21 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu. Aliongezea kwamba Mikopo hiyo imetolewa kwa mujibu wa sheria inayogusa mikopo ya Halmashauri inayotokana na makusanyo ya ndani ambapo Halmashauri zinapaswa kutenga asilimia 10% ya mapato yake ya ndani yanayotokana na vyanzo vyake kwa ajili ya kukopesha vikundi vya Wajasiriamali vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Mkurugenzi akisoma taarifa fupi ya mikopo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Karim Ali alisema kwamba vijana wameshukuru kwa kukopeshwa pikipiki kwani itawasaidia kuinua uchumi wao na kwamba watarejesha mkopo huo kwa muda muafaka waliolekezwa.
Vikundi vya pikipiki vilivyopata mkopo huo ni vikundi vya vijana wa kikundi cha Tumeungana Bodaboda kutoka Kata ya Majengo Pikipiki 4, Kikundi cha UWAMI kutoka Mtama Pikipiki 4, na Kikundi cha Vijana na Maendeleo Namupa Pikipiki 3. Pikipiki hizo 11 zina thamani ya Tshs. 27,500,000/= lakini pia vikundi vya wanawake 10 vilipokea kiasi cha Tshs. 27,100,000/= pamoja na vikundi 3 vya walemavu vilipata Tshs. 5,000,000/= na kwamba Vikundi hivyo 3 vinawakilisha vikundi vingine 21.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.