Ndugu Wenceslaus Mbilango Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, jana tarehe 5 Aprili 2024 aliongoza Sherehe ya Uzinduzi wa kampeni ya usafi na mazingira na ujenzi wa vyoo bora katika kata ya Mandwanga (Vijiji 8) na kata ya Mnara (Vijiji 2), Kampeni hiyo inayofadhiliwa na Kanisa la Angalikana Dayosisi ya Masasi kupitia Shirika la World Vision Tanzania, inalenga kuwafikia wananchi wote wa vijiji 10 ili kuwezesha kujenga na kutumia vyoo bora na kunawa maji na sabuni kwa maji tiririka baada ya kutumia choo. Kampeni hiyo iliyozinduliwa katika kijiji cha Chiuta inakadiriwa kuwafikia wananchi zaidi ya 27,000.
Katika uzinduzi huo, Ndugu Elvan Limwagu Afisa Afya wa Halmashauri alielezea na kusisitiza wananchi kujenga choo bora kwa kuzingatia sifa tano ambazo ni: Sakafu inayosafishika, jengo imara lenye kuta pande zote nne, paa lililoezekwa vizuri, mlango imara unaotunza usiri na Mfuniko kwa vyoo vya shimo. Pia aliongeza kuwa lazama kila choo kiwe na kifaa cha kunawia mikono kwa maji tiririka ili kuwezesha kunawa mikono baada ya kutoka chooni.
Wakati huohuo Afisa Mradi na mwakilishi wa Kanisa la Angalikana Bwana Victor William alisema kuwa Kampeni hii inafanyika ili kusaidia juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa kusambaza maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya vyoo katika shule na zahati zilizopo ndani ya eneo la mradi na kubadilisha mitazamo ya jamii hasa katika kubadili tabia za usafi wa mazingira.
Mgeni Rasmi Ndugu Mbilango alieleza kuwa Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dakta Samia Suluhu Hassan inatumia gharama kubwa hili kupambana na magonjwa yanayotokana na jamii kutotumia choo bora, hivyo wananchi waunge mkono kampeni hiyo kwa kujenga vyoo bora na kuvitumia. Alimalizia kwa kuwakumbusha Kauli mbiu mbalimbali zinazotumika ambazo ni "MTU NI AFYA, USAFI NI USTAARABU, USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO, USAFI WA MAZINGIRA NI USALAMA WA TAIFA, JENGA CHOO BORA SASA"
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.