Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Exaud Kigahe akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Wilayani Lindi tarehe 28 Agosti 2021 katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa alipokuwa akizungumza na Maafisa Kilimo na ushirika, Wadau mbalimbali wa kilimo, wawakilishi wa Vyama vya Msingi pamoja na wakulimwa wa zao la Korosho. Lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unavofanya kazi, faida pamoja na kusikiliza changamoto zitokanazo na Mfumo huo ili kuzipatia ufumbuzi yakinifu. Aidha alipata nafasi ya kusikiliza michango mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa kikao hicho.
Miongoni mwa wajumbe hao ni pamoja na Werner Chiwembi mkulima wa zao la Korosho Halmashauri ya Wilaya ya Mtama aliyeeleza kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali lakini kuna faida nyingi za Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ikiwa ni pamoja na uhakika na usalama wa upatikanaji na utunzaji wa fedha mara baada kuuza mazao huku akiongeza kuwa Mfumo huo umekuwa chachu ya mafanikio ya wakulima wengi kwani unasaidia katika harakati za kusomesha watoto pamoja na kutunza familia na Taifa kwa ujumla. Ametoa ushauri kwa viongozi kuwa Mfumo huo hauna budi kuendelea ikiwezekana hata kwa aina nyingine ya mazao kama vile mbaazi na mahindi.
Kwa upande wa mwakilishi wa NBC Lindi Ndg. George Malibiche alieleza manufaa yanayopatikana kupitia Mfumo huo ikiwa ni pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya wakulima wanaofungua akaunti mpya kwenye benki hiyo, kutanua wigo wa utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali kwa kutumia mawakala lakini pia Mfumo umepelekea Benki hiyo kubuni mbinu mpya za bidhaa na huduma kama vile mikopo kwa wakulima, bima za wakulima pamoja na mpango wa kuanzishwa kwa akaunti maalumu za wakulima.
Naye Diwani Viti Maalumu Tarafa ya Mtama Mh. Mariamu Kharifa amemuomba Naibu Waziri kuwekeza zaidi kwenye viwanda kwani ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kuna maeneo pamoja na malighafi ya kutosha kwa uendeshaji wa shughuli za viwanda ikiwemo zao la Korosho pamoja na Miwa na kwa kufanya hivyo kutapelekea maendeleo ya mtu mmojammoja na Taifa kwa ujumla.
Akitolea ufafanuzi wa michango mbalimbali iliyowasilishwa na wajumbe wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mh. George Kigahe amesema kuwa atahakikisha anatoa hamasa katika uwekezaji wa ndani ili kuinua na kuikuza sekta ya viwanda na biashara. Vilevile ametoa maelekezo kwa viongozi wa vyama vya msingi kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao mapema iwezekanavyo ili kudhibiti uuzaji holela wa mazao huku akisisitiza zaidi kuhusiana na suala la uadilifu kuanzia ngazi ya wakulima hadi viongozi wa Ushirika pamoja na Vyama vya Msingi kwa kuzingatia ubora na usafi wa mazao pindi yanapofikishwa ghalani kwa hatua ya uuzaji na kwamba kwa kufanya hivyo kutapelekea ushindani mzuri wa soko la kitaifa na kimataifa. Sambamba na hilo, Mh. Kigahe amewataka wakulima kuhakikisha wanakuwa na hati za mashamba yao ili kurahisisha zoezi la upatikanaji wa Mikopo lakini pia ni lazima wahakikishe wanalipa madeni ya mikopo hiyo kwenye Mabenki husika. “ naomba nisisitize hili ndugu zangu wa Lindi tusikwepe kulipa madeni lakini tuitumie kwa usahihi sio Umekopa kwa ajili ya kupulizia mikorosho lakini wewe unakwenda kupulizia nyumba ndogo; TUTUMIE MIKOPO YETU KWENYE MALENGO TULIYOKOPEA”
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.