Wawezeshaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kutoka ngazi ya Taifa, Agosti 30, 2021 wametoa Mafunzo ya kutoa huduma za kitaalamu kwa jamii katika utekelezaji wa Miradi ya kutoa Ajira za Muda kwa Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia wasimamizi wa Miradi kutoka Vijiji 69 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa lengo la kujenga uelewa katika utekelezaji wa Miradi hiyo. Mafunzo hayo yalifunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Mh. George Mbilinyi katika Ukumbi wa Mikutano.
Akifungua mafunzo hayo yaliyoambatana na Usomaji wa hotuba kwa washiriki wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Mh. George Mbilinyi amesisitiza zaidi kuhusu uaminifu na uadilifu katika utekelezaji wa Miradi hiyo “Napenda kuwasisitiza kuwa waadilifu tunapoenda kuanza utekelezaji wa miradi hii, tukafanye kazi kwa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili tufikie malengo ya serikali kupitia kipini cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF ya kupunguza umasikini na kuchochea ukuaji wa uchumi . Ni imani yangu kwamba mtasimamia miradi hii kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia miongozo na maelekezo mtakayopewa katika mafunzo haya. Sitarajii kusikia kwa msimamizi yeyote katika eneo lake la kazi kunakuwa na mradi uliofanywa chini ya kiwango au mradi usiofanana na thamani ya fedha, mimi mwenyewe kupitia maafisa wangu tutakuja kuwakagua ili tutumie vizuri rasilimali fedha na kufiki malengo yetu, hivyo hatua kali zitchukuliwa kwa msimamizi yeyote atakayefanya kinyume na maelekezo mtakayopatiwa”. Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
Sambamba na hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri alichukua fursa hiyo kuwakumbusha washiriki wa Mafunzo hayo kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa UVIKO19 kwa kufuata hatua mbalimbali za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo pindi watakapokuwa katika maeneo yao ya utekelezaji wa Miradi hiyo.
Kwa upande wake Afisa ufuatiliaji wa TASAF ambae pia ni mwezeshaji kitaifa wa mafunzo hayo Ndg. Tumain Michael Yanai, ameelezea maana ya dhana ya Miradi ya Ajira za Muda kwamba ni kazi zinazofanywa na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini kwa muda husika na kulipwa ujira, huku akitoa malengo ya Miradi hiyo ikiwa ni pamoja na kuziwezesha kaya masikini kujipatia kipato, kupata miundombinu itakayonufaisha Walengwa na jamii kwa ujumla pamoja na kuongeza ujuzi wa utendaji wa shughuli mbalimbali katika jamii.
Naye mwezeshaji wa Mafunzo Kitaifa wa Miradi ya Ajira za Muda , ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya jamii Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Ndg. Sky Thomas amewasa washiriki kutojihusisha na Rushwa wakati wa usimamizi wa miradi hiyo “Tukafanye kazi kwa moyo wa kujitolea kwani tunatamani Miradi ya awamu hii iwe yenyekufanana na thamani ya fedha, ubora, pamoja na kiwango kinachotakiwa. Tusiwe watu wa kupokea rushwa katika ukaguzi wa utekelezaji na hatutegemei katika Wilaya ya Mtama kuwepo kwa udanganyifu kwani hupelekea Miradi mbalimbali kutekelezwa chini ya kiwango, hivyo basi ni muhimu kujiridhisha kwamba Mlengwa wako amekamilisha kazi ya siku husika”. Alisema Sky Thomas.
Mafunzo hayo yanayotarajiwa kumalizika Septemba 2, 2021 yatakua ni chachu ya Mafanikio kwa Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini, lakini pia ni urahisishaji wa utekelezaji kupitia wawezeshaji wa Miradi ya kutoa Ajira za Muda zitakazodumu kwa muda wa Miezi 6 .
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.