Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Ndg. George Emmanuel Mbilinyi jana Oktoba 14 2021 ameongoza kikao cha mazungumzo na baadhi ya wawakilishi wa wazee wa Mtama ikiwa ni ishara ya kumuenzi aliyekuwa Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwl. Julis Kambarage Nyerere lakini pia kujitambulisha rasmi kwa wazee hao. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya Mh. Othmani Hongonyoko, wakuu wa Idara mbalimbali, Madiwani pamoja na watendaji wa Kata na Vijiji vya Mtama na Majengo.
Ndugu Mbilinyi amewaomba wazee hao kutoa ushirikiano wa kiutendaji ili kufikia lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi huku akiwahimiza kuwahamasisha vijana wao kujitolea kwenye Miradi mbalimbali ya kimkakati. Pamoja na hilo, Mkurugenzi huyo amewaomba wazee hao kuondoa tofauti za kiitikadi za Siasa na badala yake wajikite zaidi katika kidumisha na kuendeleza amani, upendo na mshikamano ndani ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Wazee hao pia walipata nafasi ya kutoa hoja zao ambapo kwa ujumla wametoa pongezi kwa Mkurugenzi huyo kwa kuwapa thamani kubwa ya kuwaita na kuzungumza nao lakini hawakusita kutoa changamoto na kero zao ikiwa ni pamoja na uchache wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya . Sambamba na hilo wameahidi kutoa ushirikiano katika ujenzi wa Mtama mpya kwani ni matamanio yao ya muda mrefu kuona maendeleo ndani ya Halmashauri hiyo.
Akitolea ufafanuzi wa tatizo la uchache wa dawa, Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Dismas Masulubu amesema kuwa kukamilika kwa Mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Mtama kutarahisisha upatikanaji wa dawa zitakazotibu magonjwa ya wazee kwani dawa hizo zinatolewa kulingana na ngazi ya kituo cha huduma na ukubwa wa tatizo. Aidha amewathibitishia kuwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) tayari imesambaza dawa kwa asilimia 82% hivyo basi changamoto hiyo imetatuliwa.
Mkurugenzi akiwa kwenye kikao na wananchi wa Pangatena
Awali ya hapo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama alikutana wa wananchi wa Hingawali, Njonjo na Pangatena kwenye Mkutano uliofanyika Kata ya Pangatena uliolenga kusikiliza changamoto pamoja na kuondoa migogoro na migongano baina ya wananchi wa Kata hiyo. Ametoa maelekezo kwa watendaji wa Vijiji na Kata kutatua matatizo yanayojitokeza kwenye maeneo yao ya kazi na sio kusubiri mikutano ya viongozi wa ngazi za juu itakapofanyika. "Njia nzuri ya kutatua migogoro ni kuanza kushughulika nayo kwenye ngazi za chini". George Mbilinyi. Vilevile amewaelekeza watendaji hao kuwatumia wazee wa vijiji pindi wanapohitaji kupunguza migogoro mbalimbali.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.