Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kupitia Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) imeendeleza zoezi la ugawaji dawa (kingatiba) kwa mwaka 2021 ili kuhakikisha jamii inaondokana na athari zitokanazo na magonjwa hayo ikiwa ni magonjwa ya Matende, Mabusha na Minyoo ya tumbo .
Kwa awamu hii zoezi la ugawaji dawa lilianza rasmi tarehe 24 Agosti 2021 kupitia watumishi wa afya kwa kushirikiana na Viongozi mbalimbali wa ngazi ya vitongoji, vijiji, kata na Wilaya. Pia watumishi wa afya ngazi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati wa Majimbo ya Mtama na Mchinga walitumia utaratibu wa kupita nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wanajamii wote wanafikiwa na huduma hiyo. Zoezi hilo lilikamilika tarehe 27 Agosti 2021 na kufanikiwa kufikia zaidi ya asilimia 80% ya Walengwa waliokusudiwa.
Awali ya hapo, Idara ya afya iliratibu Mafunzo kwa watumishi wa afya 112 kutoka kwenye vituo 56 pamoja na Wagawa dawa 1600 ngazi ya vitongoji ili kuwajengea ujuzi zaidi wa namna ya utoaji wa dawa hizo kwa Walengwa pamoja na matumizi sahihi ya fimbo za kupimia urefu, rejesta na vitendea kazi vya zoezi hilo. Mafunzo hayo yalitolewa katika vituo vitano tofauti ambapo Msimamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg. Nicholas Venance alishiriki na kusifu uratibu mzuri wa zoezi hilo.
Kingatiba zilizotolewa kwa wananchi ni dawa za kutibu Matende na Mabusha (Mectizan) pamoja na dawa za Minyoo ya tumbo (Albendazole). Mratibu wa NTD Wilaya Ndg. Elvan J. Limwagu anazidi kuwasisitiza wananchi kuwa dawa hizo zipo za kutoosha katika vituo vya kutolea huduma za afya na kwamba hazina athari yoyote kwa watumiaji.
KINGA NI BORA KULIKO TIBA
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.