Ikiwa ni katika muendelezo wa vikao kazi mbalimbali , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Ndg. George Emmanuel Mbilinyi Jana tarehe 1 Novemba 2021 amekutana na kuzungumza na Wenyeviti wa Vijiji vyote vya Halmashauri, katika kikao kazi hicho alihudhuria pia Mhe, Athumani Hongonyoko –Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Lindi pamoja na baadhi ya wataalamu wa Idara na vitengo mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.
Dhima kuu ya kikao hicho ni kujitambulisha pamoja na kutoa taarifa ya mapokezi ya Miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania Mh. Mama Samia Suluhu Hassan ambayo ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Tarafa ya Mtama, Fedha za miradi ya Maji, pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo kwa shule za Msingi na Sekondari lakini pia kugawa vyeti vya Hati ya usajili wa Vijiji kwa Wwnyeviti hao.
Kwenye maelekezo ya namna ya usimamizi wa Miradi hiyo, Mkurugenzi amewataka Wenyeviti hao kusimamia kwa uzalendo na uaminifu mkubwa kwani miradi hiyo inakwenda kuwanufaisha wananchi wote katika maeneo mbalimbali, pia amewahimiza kutumia rasilimali zilizopo kama vile mawe, mchanga, kokoto na rasilimali watu ili kupunguza gharama za ujenzi kwenye miradi hiyo.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji (W) aliwasisitizia Wenyeviti hao kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kasi na kuhakikisha inakamilika kwa wakati huku wakizingatia viwango na ubora unaoendana na fedha zilizotolewa na kuongeza kuwa ni lazima wakafanye kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu na watendaji wa vijiji, kata pamoja na kamati za ujenzi kwa kushauriana, kukosoana na kurekebishana kwa pamoja ili kufikia malengo na kuiendeleza Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Sambamba na maelekezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji (W) alipata nafasi ya kutoa rai kwa Wenyeviti hao kutoruhusu wahamiaji pamoja na wafugaji kuingia kwenye vijiji vyao kiholela na badala yake watumie taratibu na sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima kati ya wafugaji na wakulima “maeneo mengi sana Tanzania hii tunapata shida kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji, musikubali kupokea hongo na kuruhusu wafugaji waingie kwenye maeneo yenu na kwamba kwa kufanya hivyo mutasababisha matatizo makubwa katika jamii kwani sisi tumezoea kuishi kwa amani na wakulima wetu. Kama wanahitaji maeneo lazima wafuate taratibu na pindi zitakapokamilika matangazo yatatolewa lakini kwa sasa hatuna maeneo kwa ajili ya wafugaji” George Mbilinyi Mkurugenzi Mtama.
Mwisho kabisa alizungumzia suala la mapato na kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuwa viongozi na mabalozi wazuri kwa kuhakikisha mashine za kukusanyia mapato (POSS) zinafanya kazi kikamilifu na wasiruhusu watu kukwepa kulipa ushuru ili kuinua mapato ambayo yatakuwa chachu ya maendeleo ndani ya Halmashauri yetu ya Mtama.
Kwa niaba ya Wenyeviti waliohudhuria kikao hicho, Ndg. Shabani Ally Jalasi ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mihogoni Kata ya Mtama alitumia fursa hiyo kumpongeza Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya miradi hiyo huku akitoa wito kwa wajumbe kwenda kusimamia kikamilifu ili kuziunga mkono jitihada hizi za Serikali ya awamu ya sita. Aidha, alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama kutokana na kutambua thamani na umuhimu wa Wenyeviti wa Vijiji huku akiahidi kuwa maelekezo yaliyotolewa wameyapokea kwa lengo la kuyafanyia kazi. “ tunaenda kushirikisha jamii kwa kutumia vikao mbalimbali vya uhamasishaji ili wananchi wajitokeze kwa wingi kujitolea kwenye miradi hii ili ikamilike kwa wakati”. Shabani Jalasi Mwenyekiti wa Kijiji cha Mihogoni.
Katika kuhitimisha maagizo yake Mkurugenzi aligawa vyeti vya Hati ya usajili wa Vijiji kwa Wenyeviti na kuwaeleza kuwa ataandaa ratiba ya kuendesha mikutano ya hadhara kwa wananchi katika vijii vyote vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, ‘Mtama kwanza kwa Maendeleo’.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.