Kutokana na kuwepo kwa tatizo la usafiri, changamoto inayosababisha Maafisa uvuvi na mifugo ngazi ya Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kushindwa kuwafikia wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa pikipiki mbili Wilayani humo kwa lengo la kuboresha huduma za ugani na kurahisisha namna ya kuwafikia wananchi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa pikipiki hizo Afisa Mifugo Kata ya Sudi Bi. Jafarani Ally Mohammed, ameishukuru Serikali kupitia Wizara hiyo kwa kumaliza tatizo la usafiri hususani kwenye Kata yake huku akiongezea kuwa kutokana na uhaba wa usafiri, Idara ya Mifugo na Uvuvi ilishindwa kutekeleza majukumu kwa weredi na kiwango cha juu, hivyo basi kupatikana kwa pikipiki hizo zitakwenda kurahisisha utendaji kazi kwa wakati na ufanisi kwa kuyafikia maeneo yasiyofikika kwa urahisi na kuweza kufanikiwa kudhibiti shughuli za uvuvi haramu lakini pia kutoa elimu pamoja na huduma mbalimbali kwa wafugaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga wakati akikabidhi pikipiki hizo alisema kuwa awali katika Halmashauri ya Mtama kulikua na tatizo la magonjwa kwa upande wa Mifugo na uvuvi haramu kwa sababu Maafisa hao walikua wanashindwa kuwafikia wafugaji kwa wakati lakini pia kufanya doria za usiku ambapo amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo wa hali ya juu.
Aidha Ndemanga alieleza kwamba kupatikana kwa pikipiki hizo zinakwenda kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za mifugo, kutoa elimu za ufugaji bora kwa wafugaji pamoja na kudhibiti utokeaji wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama Ndg. George Mbilinyi ameishukuru Wizara ya Mifugo kwa kupeleka pikipiki hizo hali inayotajwa kwenda kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia Idara ya Mifugo kwani wataalamu wataweza kuvifikia kwa haraka vyanzo vya mapato hususani wakati wa mauzo ya samaki.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi pikipiki 300 kwenye Halmashauri 184kwa awamu ya kwanza nchini ambapo Halmashauri ya Mtama imepokea pikipiki mbili zitakazohudumia Kata ya Sudi na Kiwalala.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.