Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Ndg. Gilbert Kalima tarehe 16/09/2021 amekamilisha ziara ya siku mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na kufanikiwa kutembelea na kukagua Miradi mbalimbali ya maendelea ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu aliambatana na uongozi wa Chama ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mtama Mh. Nape Nnauye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtama Mh. Yusuph Abdallah Tipu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. George Emmanuel Mbilinyi.
Miongoni mwa Miradi aliyoitembelea ni pamoja na Mradi wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Kata ya Kiwalala uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.8, Mradi wa umaliziaji wa maabara ya sayansi shule ya sekondari Mahiwa uliogharimu kiasi cha shilingi 40,000,000/=, Mradi wa Maji wa Namupa unaofadhiliwa na Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Masasi unaotumia zaidi ya shilingi 400,000,000/= pamoja na Mradi wa Barabara ya Mahakama ya Mwanzo Mtama uliotumia shilingi 296,690,000/= kwa hatua ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo. Aidha Katibu Mkuu alipata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na Wanachama wa CCM kupitia mashina yao ya Chama ili kuibua changamoto zinazowakabili ambapo alitembelea Shina namba sita la Naijongolo Kata ya Nyangao pamoja na Shina namba nne la Msiondoke Kata ya Mtama ndani ya Jimbo la Mtama.
Akitolea ufafanuzi kwa changamoto zilizowasilishwa na Mkuu wa shule ya sekondari Mahiwa Mwl. Onoratha Tarimo kuhusu uhaba wa maji, ukosefu wa zahanati pamoja na usafiri; Mbunge wa Jimbo la Mtama Mh. Nape Mosses Nnauye amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi 75,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa zahanati itakayohudumia wanafunzi wa shule hiyo pamoja na jamii inayowazunguka, vilevile amewahakikishia wanafunzi hao kupatikana kwa gari la shule ili kurahisisha usafiri wa wagonjwa. Aidha ametoa shukrani kwa Kanisa la Anglikan kwa kufadhili Mradi wa maji utakaowanufaisha wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wananchi kwa ujumla.
Kadharika, Mh. Nape alitolea ufafanuzi kuhusu uhaba wa maji kutoka kwa wanachama wa Shina namba sita la Naijongolo Kata ya Nyangao huku akisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi wa maji wa Chiuwe ili kusambaza huduma ya maji katika Kata ya Nyangao pamoja na Makao Makuu ya Halmashauri.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Ndg Gilbert Kalima alitoa pongezi kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Halmashauri hiyo lakini pia amewahakikishia wananchi kuwasilisha kwenye ngazi ya Taifa changamoto zilizotolewa katika maeneo aliyotembelea kwa utekelezaji zaidi. Ametoa wito kwa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi kutoa hamasa na elimu kwa wananchi kwa lengo la kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Ziara hii ya Sekreterieti ya Chama Chama Cha Mapinduzi Taifa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mama Samia Suluh Hassan kutembelea wanachama ngazi za mashina pamoja na matawi ili kuibua changamoto mbalimbali za wananchi na kuzifanyia kazi na kuweza kuimarisha Chama.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.