Vijiji kumi vya Kata ya Nyangao na Namangale vimeendesha uhakiki binafsi wa hali ya uboreshaji wa vyoo katika kaya. Vijiji hivyo vimetekeleza kazi hiyo kwa uwezeshwaji wa Shirika lisilokuwa la serikali la Heart to Heart Foundation linalofanya kazi na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Shirika hilo linaunga mkono kampeni ya Nyumba ni Choo katika kata mbili, kata ya Nyangao na kata ya Namangale ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama. Tangu mwezi Machi 2023 shirika la HtHF limejikita katika kata hizo mbili kutekeleza afua ya Kampeni ya usafi wa mazingira ili kupambana na kupunguza magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na uchafu wa choo kama vile kuhara, kuhara damu, homa ya matumbo na kipindupindu.
Heart to Heart Foundation limesaidia sana jamii ya kata hizo kujua mapungufu waliyokuwa nayo na hivyo kupitia elimu juu ya umuhimu wa choo bora iliyosisitizwa, wananchi sasa wanaelewa choo bora lazima ijengwe kwa kuzingatia sifa tano muhimu ambazo ni sakafu inayosafishika, jengo imara lililojengwa kwa miti na udogo au tofali, mlango unaofungika na unaotunza siri, paa lililoezekwa vizuri na kuzuia mvua isiharibu shimo la choo na mfuniko usiopitisha harafu na wadudu kama vile inzi na mende.
Katika zoezi hilo Afisa Afya wa Halmashauri Bwana Elvan Limwagu akiwa na timu yake, wakishirikiana na Mratibu wa Shirika la HtHF Bwana Eston Waliha walifanya ufuatilia wa mikutano ya uhamasishaji iliyofanyika ngazi ya vitongoji kwa lengo la kusisitiza kaya zote ndani ya vijiji vya kata hizo ziwe na vyoo bora kabla ya uhakiki. Aidha Afisa Afya wa Halmashauri alitoa pongezi kwa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji kwa ushirikiano wao na wananchi na kuwezesha kufikia asilimia 70 ya kaya zote kuwa na vyoo bora ndani ya kipindi cha utekelezaji huo. Afisa Afya Limwagu amewataka viongozi hao kuongeza bidii, juhudi na hamasa kufikia lengo la mradi huo ifikapo Febuari 2024.
Aidha Mratibu wa Heart to Heart Foundation ndugu Eston Waliha amebainisha kuwa Mafanikio ya mradi huo katika vijiji vya kata hizo utawezesha kazi za mradi huo kupanuliwa na kuzifikia kata zingine zaidi hapo mwakani lengo likiwa ifikapo mwaka 2026 kaya zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama viwe na vyoo bora na kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuongeza na kuimarisha utoaji wa huduma za afya zilizo bora.
Sambamba na ilo Ndugu Limwagu aliongeza kuwa mradi huo umefanikiwa kwa
kupunguza magonjwa yanayozuilika kwa matumizi sahihi ya choo na unawaji wa mikono baada ya kutoka chooni na hivyo idadi ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali kupungua. Aliwataka wananchi wote kutopuuza elimu wanayopata na kwamba waendelee kuhamasishana kujenga vyoo bora ili kutimiza lengo la mradi huu, pia HtHF limesaidia kujenga vyoo vinne vya mfano (choo moja kwa kila kijiji) katika kijiji cha Mahiwa, Namangale, Mawilo na Mtakuja II kwa kaya nne zisizojiweza ili wananchi waone na kuiga. #USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.