Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Ndg. George Emmanuel Mbilinyi kufuatia Mpango mkakati wa wananchi wa Kijiji cha Mtualonga kukubaliana kuchangia fedha shilingi 3,000/= na matofali 2 ya nchi 6 yenye kiwango na ubora sawa ili kuendeleza ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata itakayojengwa kwenye kijiji cha Tulieni kwa lengo la kupunguza hadha ya usafiri inayowakumba watoto wao wakati wanapohitaji kwenda shuleni.
Mkurugenzi alikutana na wananchi wa kijiji hicho kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 2/11/2021 na kutoa maelekezo ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa kituo shikizi chenye vyumba 2 vya madarasa kijiji cha Nammeda. Katika mkutano huo Mkurugenzi aliambatana na timu ya Wataalamu wa Halmashauri (CMT) kutoka idara mbalimbali ambao walipata nafasi ya kujibu na kutolea ufafanuzi wa hoja na changamoto zilizotolewa na wananchi hao.
Kabla ya kusikiliza hoja, maoni na changamoto Mkurugenzi aliwataka viongozi kwa ngazi ya Kijiji na Kata kuhakikisha Mradi huo unasimamiwa kwa umakini, uzalendo na ushirikiano na wanajamii. Aidha amesisitiza kutumia rasilimali zilizopo ili kupunguza gharama za ujenzi. Sambamba na hilo, Mkurugenzi huyo aliwaomba wazee wa kijiji hicho kuunda baraza la wazee litakalojikita katika kutoa ushauri, kukosoa pamoja na kurekebisha makosa yanayofanywa na viongozi mbalimbali. Aliwaeleza kuwa wazee wa kijiji wana nafasi ya kukutana na kutoa mawazo na ushauri pindi wanapoona kuna dosari katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, wazee hao wamemuhakikishia kuwa kupitia baraza watakaloliunda watafanya tathimini ya maendeleo ya miradi mbalimbali kila baada ya miezi 3 ili kuchochea suala la uwajibikaji katika shughuli mbalimbali kwenye jamii.
Katika kikao hicho, wananchi walieleza kero zao ikiwa ni pamoja na licha ya kukatwa fedha kwa ajili ya bima ya afya iliyoboreshwa (ICHF) lakini bado hawajapata huduma hiyo pia walihoji kuhusu mikopo ya vikundi kutotolewa kwa wakati.
Akitolea ufafanuzi wa hoja ya bima ya afya iliyoboreshwa, Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Dismas Masulubu amesema kuwa kutokana na changamoto ya urekebishaji wa kadi za awali ilipelekea kuchelewa kwa zoezi la uandikishaji lakini kwa sasa kadi hizo tayari zimeshapatikana na timu ya wasajili inaendelea na kazi hiyo hivyo basi kwa mwanchi yeyote ambaye hajapata huduma hiyo anatakiwa kujitokeza kujisajili siku ya tarehe 6/11/2021 wakiwa wamekamilisha kaya zao huku akifafanua kuwa bima hizo zitafanya kazi kwa mwaka mzima kuanzia siku ya kujiandikisha na kwamba bima hizo zinatumika kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya vya serikali pekee.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Sharifa Tapalu alitolea ufafanuzi wa upatikanaji wa mikopo ambapo alisema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi vya vijana wenye umri kuanzia miaka 18-33, wanawake pamoja na watu wenye ulemavu hivyo basi ili vikundi hivyo viweze kupata mikopo ni lazima viwe na shughuli maalumu ya kijasiliamali ili fedha hizo ziendeleze miradi hiyo. Aidha alisistiza umuhimu wa kulipa fedha za mikopo ya awali ili kuisaidia Halmashauri kuendelea kutoa fedha kwa vikundi vingine.
Naye Muweka Hazina wa Halmashauri CPA Asha Msangi alitumia fursa hiyo kusisitiza juu ya suala la ukusanyaji wa mapato kwa kuendelea kulipa ushuru lakini pia amewataka wananchi hao kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake katika kusimamia na kumsaidia Mtendaji wa Kijiji katika kufuatilia watu wasiolipaa ushuru wa shughuli zao za kiuchumi.
Mtendaji wa Kata ya Longa Bw. Oscar Daudi Millanzi alitoa shukurani kwa Mkurugenzi kwa kupeleka nguzo za umeme kwenye Mradi wa maji wa Mtualonga na kwamba kwa sasa huduma ya maji inapatikana katika kijiji hicho.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.