Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama George Mbilinyi leo tarehe 25 Agosti 2021 ametoa vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira ya miguu kwa timu ya mpira wa miguu ya Mtama Boy's kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na vijana hao katika kuendeleza michezo katika Halmashauri hiyo. Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo imefanyika katika maeneo ya Halmashauri na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mh. Othmani Ongonyoko, Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Yusufu Tipu, Afisa michezo Masoud Elewa pamoja na mdau wa michezo Selemani Mathew.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Mbilinyi amewataka vijana hao kuwa na tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara kwani yatawasaidia kufanya vizuri katika mpira wa miguu, na kusisitiza kuwa mazoezi ni afya, michezo ni burudani lakini pia ni fursa ya ajira. Aidha Mbilinyi ameahidi kuwa Halmashauri yake itaendelea kulipa kipaumbele suala la michezo na kuendelea kutoa mchango katika sekta hiyo kwani kuna vijana wengi wana vipaji vya kucheza mpira wa miguu hata hivyo hawajapata fursa ya kuonekana kutokana na changamoto ya vifaa jambo ambalo linasabisha kushindwa kuonesha vipaji vyao. “tumepata mipira hii saba pamoja na vifaa vingine vya kuanzia lakini tunatarajia ndani ya wiki hii tutakamilisha vifaa vilivyopungua. Lengo letu ni kutengeneza timu imara ya Mtama ambayo ni Mtama Boys itakayounda timu ya wachezaji ambao wataenda kusaidia timu ya Namungo ili tuweze kupunguza makali ya kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi. Michezo ni "platform" na kiungo muhimu kati ya serikali , Chama pamoja na wananchi hata Mwalimu Nyerere alitumia sekta ya michezo katika harakati za kudai uhuru lakini pia michezo ni sehemu nzuri ya kufikisha ujumbe kwa jamii hivyo tujikite zaidi katika sekta hiyo. .Sasa hivi mpira unalipa sana umesaidia vijana wengi wa Kitanzania kunufaika Kutokana na michezo ,hivyo natumaini mipira hii inakwenda kusaidia kuibua vipaji vya vijana katika halmashauri hii na kuweka kupata timu itakayoshiriki ligi daraja la kwanza ikiwezekana ligi kuu.” amesema Mbilinyi. Pia Mh. Mbilinyi ameahidi kuibua vipaji na michezo mingine ikiwemo mchezo wa bao ndani ya Halmashauri ya Mtama.
Kwa upande wake mdau wa michezo Selemani Mathew amempongeza Mkurugenzi huyo kwa kutoa vifaa huku akitoa wito kwa wadau wengine wapenda michezo kujitokeza kuwaunga mkono kwani bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Jezi,viatu nakadhalika.
Akitoa shukurani mara baada ya kupokea vifaa hivyo Nahodha wa timu hiyo Twaha Kabongo amemshukuru Mkurugenzi na kuahidi kuwa atahakikisha kuwa vifaa hivyo watavitunza na kuvitumia ipasavyo kwa lengo lililokusudiwa na kuongeza kuwa hawatomuangusha kwani dhamira yao ni kuona vijana wengi miongoni mwao wanapata nafasi ya kuchezea Ligi Kuu Tanzania Bara na hata nje ya Nchi.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.