Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama Ndg. George Emmanuel Mbilinyi amekiri kutoridhishwa na hali iliyopo kwenye kituo cha mabasi Mtama kutokana na kukosa vigezo na hadhi kwani kituo hicho kwa sasa hakina sehemu za chakula wala maeneo ya kupumzika abiria.
Amezungumza hayo jana tarehe 29/10/2021 kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Robo ya Kwanza 2021/2022 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri wakati akitolea ufafanuzi wa hoja iliyotolewa na diwani wa Kata ya Mnara Mh. Athumani Mpole kuhusu hali ya kituo hicho. Amesema kuwa licha ya stendi hiyo kukusanya mapato ya Tsh. 10,000,000/= kwa mwezi lakini bado huduma zinazopatikana haziridhishi hivyo ametuma wataalamu wake wa Halmashauri kwenda kujifunza kwenye stendi ya Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara ili wafanye maboresho ya kituo hicho.
Mkurugenzi amesema kuwa Kuhusu suala la ushirikishwaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambalo limekuwa likilalamikiwa na Madiwani wengi kwenye Baraza hilo, Mbilinyi ataahakikisha kuwa kuanzia sasa madiwani hao watashirikishwa kila hatua ya miradi kupitia vikao mbalimbali lakini pia atafanya ushirikishwaji kwa wananchi pamoja na viongozi wa Vijiji na Kata.
" tukitaka tuirekebishe na kuijenga Mtama ni lazima tufikirie kuwa sisi ni Watanzania na ni lazima tuwe na ushirikiano baina ya Madiwani na Watumishi wa Halmashauri" Tusipokuwa na umoja na kukosa ushirikiano hatutaweza kufikia malengo yetu. Mimi nikiwa kama kiungo muhimu naahidi kwamba naenda kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja." George Mbilinyi Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.
Sambamba na hilo, Ndg. Mbilinyi amesisitiza matumizi ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo ambayo miradi inaendelea hususani Miradi ya ujenzi wa madarasa kupitia fedha za UVIKO19 ili kupunguza gharama na kuepuka ubadhirifu wa fedha huku akiongeza kuwa kwa kufanya ivo kutatoa fursa kwa wananchi kujipatia kipato kupitia shughuli za uuzaji wa malighafi ya ujenzi kama vile kokoto na mchanga.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Lindi Ndg. Thomas Safari amewataka Madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri kufanya kazi kwa umakini na umoja ili kukamilisha Miradi iliyopokelewa lakini pia kuhakikisha thamani ya fedha iliyotumika inaendana na viwango vya jengo husika.
Wajumbe wa Baraza hilo wamempongeza Mkurugenzi kwa kuonesha njia bora ya mafanikio na kuhahidi kuwa watamuunga mkono katika kila hatua ya maendeleo kwa lengo la kuleta mabadiliko ndani ya Halmashauri. "Baraza la leo tumelipokea vizuri na tuna matumaini kwa kiongozi wetu kwani asilimia kubwa ya jitihada zake zinaendana na matamanio yetu, kwaiyo nitoe wito kwa madiwani wenzangu tukasimamie majukumu katika maeneo yetu ya kazi na tuondoe matabaka kati ya watumishi na Madiwani hii itasaidia kuiendeleza Mtama yetu". Hamza Nguwachi Diwani Kata ya Nahukahuka.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.