Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 29 Septemba 2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa lengo la kutoa elimu pamoja na hamasa kuhusu umuhimu na faida ya Chanjo ya UVIKO-19. Kikao kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya Ndg. Shaibu Ndemanga ambae alikua Mgeni rasmi huku akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lindi Mh. Othmani Hongonyoko, wawakilishi kutoka Wizara ya Afya, viongozi wa Dini, pamoja na watumishi kutoka idara mbalimbali.
Katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ametoa wito kwa watumishi na wajumbe waliohudhuria kujikita zaidi kutoa hamasa kwa wananchi kuhusu Chanjo ili kuongeza idadi ya watu waliopatiwa chanjo hiyo kwa usalama wa mwananchi mmojammoja na taifa kwa ujumla huku akiwasisitiza watumishi wa Halmashauri pamoja na madereva wa bodaboda kuwa msitari wa mbele kupatiwa huduma hiyo kwa kuwa ni makundi yaliyo katika mazingira hatarishi “Mkurugenzi wahamasishe watumishi wako wachanje Afisa Elimu nyuma yako kuna walimu wahamasishe kwani huko tunakoelekea tunaweza kukosa baadhi ya mambo kwa sababu hatujachanja; chanjo hii ni salama inapatikana bure hivyo hatuna budi kuitumia. Viongozi wa Dini tumewaita hapa mtusaidie kuwaambia waumini wachanje hii ni njia sahihi na salama ya kukabiliana na ugonjwa huu wa COVID-19” .Alisema Shaibu Ndemanga Mkuu wa Wilaya ya Lindi
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri Wilaya ya Mtama Dkt. Dismas Masulubu amesema katika jitihada za kutekeleza Mpango Harakishi na Shirikishi wa chanjo, Halmashauri tayari imeshasambaza Chanjo kwenye vituo 15 na itahakikisha inafanya huduma ya mkoba ili kuwafikia walengwa katika maeneo yaliyokuwa mbali na vituo vya kutolea huduma hiyo huku akiongeza kuwa watahakikisha wanayafikia makundi yaliyosahaulika ikiwemo kundi la walemavu.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.