Mkuu wa Wilaya Lindi, Mh.Shaibu Ndemanga, amefanya mkutano kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Mbuta, kata ya Mnolela pamoja na Litipu, kata ya Nyangamara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama. Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutambulisha Mradi wa uwekezaji wa Shamba la Pamoja na Kiwanda cha Miwa kutoka kampuni ya “SJ Sugar Company” inayomilikiwa na Muhindi. Aidha, mikutano hiyo ililenga kutatua migogoro iliyojitokeza hapo awali, kati ya watumiaji wa eneo la mradi huo kutoka katika vijiji jirani vya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara.
Akitolea ufafanuzi juu ya umiliki wa eneo hilo, Mh.Shaibu Ndemanga, amesema kuwa, Mmiliki rasmi wa eneo hilo ni Serikali na kwamba kabla ya Wananchi kujishughulisha na shughuli za kilimo katika Shamba hilo, eneo lilitengwa kwa ajili ya Malisho ya Mifugo. Aidha, mkuu wa Wilaya ameongezea kuwa katika umiliki wa eneo la Mradi huo jumla ya hekari 2059.7, kati ya hekari zaidi ya 8000 ya Shamba zima ni mali ya Wilaya ya Lindi.
Pia amesema kuwa kulingana na hali ya umiliki kuwa ni ya Mikoa Miwili, Serikali imemtaka Mwekezaji huyo kabla ya kuanza rasmi shughuli za uwekezaji , kutoa “ Kifuta Jasho” kwa Watumiaji wa eneo hilo. Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya amewaelekeza Wataalamu wa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, kuanza zoezi la Utambuzi wa Watumiaji haraka iwezekanavyo ili wananchi hao wapate stahiki zao. Katika Makubaliano kati ya Mmiliki na Mwekezaji, Serikali imemtaka Mwekezaji huyo kutoa mafunzo ya Kilimo cha Miwa, kutoa Mbegu bora za Miwa pamoja na kufungua fursa za soko kwa wakulima wadogo.
Shamba hilo lipo katika mpaka wa Mkoa wa Mtwara na Lindi na lina ukubwa wa zaidi ya hekari 8000 ambapo kati ya hekari hizo jumla ya hekari 2059.7 lipo katika Wilaya ya Lindi na hekari zilizobakia zipo katika Wilaya ya Mtwara vijijini. Vijiji vilivogusa shamba hilo ni pamoja na Litipu na Mbuta katika Wilala ya Lindi, na kijiji cha Lilido kwa upande wa Mtwara
Hapo awali, Mkuu wa Wilaya, alipata fursa ya kuwapongeza Wananchi wa Kijiji cha Mbuta, kwa kuwa na moyo wa kujitolea kurekebisha barabara ya Mnolela-Mbuta na kuwahakikishia kilio cha barabara kimefika tamati kwani Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya utengenezaji wa barabara hiyo kwa kiwango cha Kifusi na Changalawe. Mh. Ndemanga, amewaeleza Wananchi wa Mbuta na Litipu kuwa Serikali imejipanga kusogeza huduma za Afya, umeme pamoja na maji na kwamba tayari Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kupitia Mpango wa Usambazaji wa Umeme ndani ya miezi 18, wapo katika hatua za awali za utekelezaji.
Vilevile, ametoa wito kwa Vijana na Wananchi wa Mbuta na Litipu, kuwa na utayari wa kutumia Umeme huo kwa shughuli za Maendeleo, pamoja na kujikita zaidi kwenye kilimo cha miwa na kuchangamkia fursa katika Mradi huo wa Uwekezaji na amewasisitiza zaidi wananchi hao kuacha tamaduni za kuuza maeneo yao kiholela.
Kwa upande wa Mmoja wa wakazi wa Mbuta Bw. Mohamedi Hamisi Mkulula , alitoa shukurani kwa niaba ya Wananchi kwa ujio na ripoti iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa, huku akiahidi kuwa wako tayari kujitolea zaidi katika ujenzi wa Zahanati ya Mbuta, kwani, tayari Kijiji kimetenga eneo na wapo katika hatua ya kutoa Michango kwa hiyari.
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.