Mkuu wa Wilaya ya Lindi Ndg. Shaibu Ndemanga leo tarehe 2/11/2021 amezindua rasmi Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtama itakayoshughulika na kusimamia huduma zinazotolewa kwenye vituo mbalimbali vya Afya. Uzinduzi huo umefanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Geoge Emmanuel Mbilinyi pamoja na baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri hiyo. Tukio hilo lilihusisha pia uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo.
Kabla ya uzinduzi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Dismas Masulubu aliwaeleza wajumbe wa bodi hiyo baadhi ya majukumu yao ikiwa ni kuhakikisha wanasimamia utoaji huduma katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali, kusimamia upatikanaji wa watumishi, miundombinu pamoja na vitendea kazi. Aidha Dkt. Dismas alitoa rai kwa wajumbe wa Bodi kuhakikisha wanaenda kupunguza vifo vya mama na mtoto lakini pia kuwa mabalozi katika uhamasishaji kwa wananchi ili waweze kupata chanjo ya UVIKO19 na chanjo za kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi ambaye pia aliwataka wajumbe wa bodi hiyo kukutana vikao vyote vya kisheria bila kujali maslahi yao binafsi, kufahamu na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza, kujua dawa zinazopelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma kama zinatolewa ipasavyo kwa walengwa, kuwa na mahusiano mazuri na taasisi binafsi zinazotoa huduma za afya, kujua mipaka ya kikazi kati ya bodi, kuchuja mambo muhimu ya kupeleka katika ngazi ya halmashauri pamoja na kupitia mirejesho inayopitishwa na halmashauri tayari kwa utekelezaji. Aidha, alitoa rai kwa wajumbe wa bodi hiyo kutojihusisha na siasa katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake wanatakiwa kusikiliza maoni ya viongozi au watu mbalimbali bila kujali itikadi zao za chama ili kuleta ufanisi katika uwajibikaji.
Nae mwenyekiti wa Bodi hiyo ambae alichaguliwa Ndg. Mohamedi Chilumba alitoa neno la shukurani kwa kuaminiwa kuwa kiongozi lakini pia alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa Bodi ya awamu hii ni ya kipekee na kwamba inakwenda kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na wataalamu wa Idara ya Afya na wananchi kwa ujumla.
Bodi ya Afya ya Halmashauri na Kamati za Afyaza Vituo vya kutolea huduma zipo kwa mujibu wa sheria ndani ya Hati Rasmi chini ya Sheria Sura Na. 287 na 288 ya Sheria ya mwaka 1993. Kufuatia sheria hiyo, wajumbe wa bodi waliochaguliwa kutoka katika vijiji vyao walifanya uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu ambapo Ndg. Mohamedi Chilumba alipita bila kupingwa huku Bi. Moza akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. Bodi hiyo itakuwa madarakani kwa muda wa miaka 3 na itafanya kazi kwenye zahanati 28, vituo vya afya 4, pamoja na hospitali 2.
Mwenyekiti wa baodi Bw. Mohamedi Chilumba akitoa neno la shukurani baada ya kuchaguliwa
wajumbe wa bodi wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Ndg. Shaibu Ndemanga na baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri
Box 328 Lindi
Sanduku la Barua: 328 Lindi Dc
Simu ya mezani: 0222061
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@lindidc.go.tz
Copyright ©2021 Mtama District Council All rights reserved.